Dar es Salaam. Mazingira yanaweza kuwa tofauti, lakini mgogoro unaoonekana kukiandama Chama cha Wananchi (CUF) unaanza kuchukua sura iliyodhoofisha vyama vingine vya upinzani vilivyokuwa na nguvu baada ya kurejeshwa kwa siasa za ushindani.
CUF inapitia kwenye kipindi kigumu kutokana na vyombo vyake vya juu kutofautiana na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ameghairi uamuzi wake wa kujiuzulu, takriban mwaka mmoja baada ya kukiacha chama hicho katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Wakati Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad anaungana na zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa vikao vyote vya juu, Profesa Lipumba anaungwa mkono na wajumbe wachache wa mkutano mkuu na kikundi cha wafuasi wake cha jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba na wafuasi wake wamepata nguvu zaidi baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kueleza msimamo wake kuwa anamtambua msomi huyo kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF, uamuzi uliowafanya waende hadi ofisi kuu za chama na kujimilikisha hadi leo.
Hali hiyo ndiyo iliyowahi kuikumba NCCR-Mageuzi iliyokuwa na nguvu kubwa baada ya nchi kurejea kwenye siasa za ushindani, lakini mgogoro mkubwa wa uongozi ulisababisha kipoteze nguvu zake.
No comments:
Post a Comment