“Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao. Mara wale watu walipomwona Yesu, wakastaajabu sana, wakamkimbilia, ili kumsalimu.
Akawauliza wanafunzi Wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?’’
Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu ambaye ana mfanya asiweze kuongea. Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.’’
Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitachukuliana nanyi mpaka lini? Mleteni huyo mvulana kwangu.”
Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.
Yesu akamwuliza baba yake, “Mwanao amekuwa akitokewa na hali hii tangu lini?’’ Akamjibu, “Tangu utoto wake. Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lo lote, tafadhali tuhurumie utusaidie.’’
Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.’’ Mara baba yake yule mvulana akapiga kelele akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!’’ Yesu alipoona kwamba umati wa watu unakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, ‘‘Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke wala usimwingie tena!”
Yule pepo mchafu akiisha kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, ‘‘Amekufa.’’ Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua, naye akasimama.
Baada ya Yesu kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi Wake wakamwuliza wakiwa peke yao, ‘‘Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?’’
Yesu akawajibu, ‘‘Hali hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba na kufunga’’ #MARKO 9:14-29
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai ewe mpendwa wangu.
Mwana wa Mungu kwanza napenda kumshukuru Mungu ambaye anaendelea kututia nguvu katika kazi yake. Nakushukuru wewe ambaye huchoki kuomba kwa ajili yetu kama nasi pia tusivyochoka kuomba kwa ajili yenu. Mungu aliye hai na mwaminifu anajua namna gani tunakesha kwa ajili yenu. Ainuliwe Mungu ambaye haachi kutuhuisha hata pale tunapokuwa tumechoka. Nami ni maombi yangu Roho wa Kristo akuhuishe roho na nafsi yako unapokuwa umechoka. Imeandikwa ‘Hata vijana huchoka na kulegea, nao vijana wanaume kujikwaa na kuanguka, bali wale wamtumainio BWANA atafanya upya nguvu zao. Watapaa juu kwa mbawa kama tai, watapiga mbio wala hawatachoka, watatembea kwa miguu wala hawatazimia. #Isaya 40:30-31
Ni maombi yetu Mungu afanye upya nguvu zako za rohoni upae juu kama tai usirudi nyuma katika jina la Yesu.
Mpendwa wangu Bwana Yesu anatuambia siri ya ajabu sana hapa kuhusu Imani na kufunga na kuomba. Kwenye #WARUMI 15:4 imeandikwa ‘kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini’. Jambo hili lililowatokea wanafunzi wa Yesu kushindwa kumtoa pepo ndani ya kijana yule aliyekuwa kwenye mateso makubwa ni mfano mzuri tu kwa kanisa la leo. Kwani ni mambo mangapi tumefeli kuyatatua kwenye kanisa? Watu wangapi wamekuja wakisumbuliwa na nguvu za pepo wachafu halafu wanaondoka bila msaada. Ushawahi kujiuliza kwanini watumishi Fulani waweze kuwasaidia watu kufunguliwa toka kwenye mateso lakini sio wewe au sio ninyi kanisani kwenu?
Mahali Fulani nilikuta kanisa moja Mchungaji amechukua mke wake kwenda kuombewa sehemu Fulani kwa kuwa yeye na kanisa lake hawaamini katika uponyaji na miujiza ya Yesu! Yamkini sisi sote kwa namna moja au nyingine tumepitia katika kufeli kushindwa kuwasaidia watu wenye shida za namna mbalimbali kwa sababu hatuamini katika uponyaji wa Yesu au hatuna nguvu za rohoni kufanya hivyo. Lakini hilo